• x1a.jpg
  • xIMG_0253.jpg
  • xIMG_0426.jpg
  • xIMG_4933.jpg
  • xk.jpg
  • xp.jpg
  • xz.jpg

HISTORIA

Historia ya shule ya Sekondari ya Seminari ya Fransalian Hekima

Jumuiya ya Wamisionari wa Mtakatifu Fransisko wa Sale ni Shirika la kikatoliki la kimataifa lililopo katika nchi 27 lenye wafuasi zaidi ya 1300. Shirika lilianzishwa mwaka 1838 nchini Ufaransa na Mtumishi wa Mungu Mheshimiwa Padri Peter Mermier chini ya mlezi wetu Mtakatifu Fransisko wa Sale. Shirika limeenea katika nchi mbalimbali barani Afrika ambazo ni Afrika Kusini, Namibia, Swaziland, Mozambiki, Chadi, Cameroon, Zambia, Malawi, Uganda, Kenya na Tanzania. Wamisionari wa shirika hili wanajishughulisha na shughuli mbalimbali za kijamii nchini Tanzania ikiwamo ufugaji, elimu na afya tangu mwaka 1988. Shirika limesajiliwa na wizara ya mambo ya ndani nchini Tanzania kwa namba 9118, linafanya shughuli zake katika mkoa wa Tabora,Morogoro,Pwani,Dar es Salaam , Shinyanga, Dodoma na Arusha. Shirika lilianza shughuli zake mkoani Arusha mwaka 2010 katika Kijiji cha Kitefu kilichopo Wilaya ya Meru. Tunatoa huduma za kijamii ambazo ni kilimo, Elimu, Afya na huduma nyinginezo kupitia taasisi ya Lumeni Christi.

Wamisionari wa Mtakatifu Fransisko wa Sale wanazo shule mbalimbali za awali, shule za elimu ya msingi, shule za sekondari na Chuo cha ufundi katika mikoa tofauti ya Tanzania. Shule za awali na elimu ya msingi zipo maeneo ya Kigurunyembe(Morogoro), Ipuli na Bukene(Tabora), Kagonwa na Isaka (Shinyanga), na  Mkuza Kibaha(Pwani). Shule za sekondari zipo Kihonda mkoa wa Morogoro na Ipuli iliyopo mkoani Tabora. Chuo cha ufundi kipo Mwakata Isaka mkoani Shinyanga.

Baada ya kutambua umuhimu wa elimu kwa Tanzania ijayo,tuliamua kuanzisha shule ya sekondari katika mkoa wa Arusha ili vijana wadogo waweze kupata elimu bora ya sekondari. Vijana ni utajiri wa Taifa. Kwa sababu hii, Shirika liliamua kuanzisha shule ya sekondari eneo la Maji ya chai ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuondoa umasikini kupitia elimu bora.

Tarehe 8/1/2018 Mheshimiwa Padri Abraham Vettuvellil, Mkuu wa shirika la Mtakatifu Fransisko wa Sale (Wafransaliani) aliibariki na kuizindua shule ya sekondari ya seminari ya Fransalian Hekima. Shule imesajiliwa na Wizara ya elimu Tanzania kwa namba ya usajili S.5013.

Shule inatoa elimu ya kiwango cha juu katika ngazi ya kidato cha Kwanza hadi cha Nne kwa wavulana na wasichana kwa dini zote. Shule ina majengo na miundombinu ya kisasa ikiwemo vyumba 12 vya madarasa, Maabara ya Biolojia, Kemia na Fizikia, Maktaba iliyosheheni vitabu mbalimbali na Bwalo lenye uwezo wa kubeba zaidi ya watu 1000. Tuna mabweni mazuri ya wavulana na wasichana.

Maendeleo ya nchi hutegemea elimu ya wananchi. Uongozi, walimu na wafanyakazi wengine wa Hekima wamejizatiti na kujikita katika kuwajenga wanafunzi wetu kuwa wananchi wazalendo wa Tanzania kwa kuwapatia Hekima na Maarifa kupitia elimu yenye maadili. Uongozi wa Shule unajali makuzi ya wanafunzi wetu kwa kutoa semina endelevu ili kuwapatia motisha na hamasa pamoja na kuwajumuisha katika shughuli mbalimbali nje na darasani ikiwemo michezo na sanaa.

MOTO WETU

“HEKIMA NA MAARIFA”

MAONO YETU

Shule ya Sekondari Fransalian Hekima inaangazia katika kupambana na kujibidisha katika ubora wa taaluma kwa ajili ya makuzi ya jumla kwa vijana na kuwajenga kuwa wananchi wazalendo na wawajibikaji watakaoijenga nchi kwa Hekima na ukarimu.

DHAMIRA YETU

Shule ya Sekondari ya Seminari Fransalian Hekima imejitolea katika kuendeleza ukuaji wa jumla,mwenendo na utu wa mwanafunzi kwa kuwapa mwongozo wa kielimu na makuzi kupitia mafunzo ya darasani na shughuli nyingine za ziada.

MAADILI YETU YA MSINGI

  • Upendo na huduma
  • Ukweli na haki
  • Uaminifu na uadilifu
  • Kujitolea na ufanisi
  • Ushirikiano na ubora

ENEO SHULE ILIPO

Shule ya Sekondari ya Seminari Fransalian Hekima ipo Maji ya Chai (Dolly Estate/Kitefu) katikati ya barabara kuu ya Arusha (25 KM) na Moshi (54KM). Ipo umbali wa mita  300 kutoka kituo cha magari cha  Maji ya Chai.

MASOMO YANAYOFUNDISHWA SHULENI

Shule inafundisha masomo ya sayansi, sanaa na biashara . Masomo yanayotolewa ni:

01. Kiswahili
02. English
03. Mathematics
04. Physics
05. Chemistry
06. Biology
07. History
08. Civics
09. Geography
10. Computer Science
11. Book Keeping
12. Accountancy
13. Bible Knowledge